Monday, November 21, 2011

Vijiji na maendeleo

Hao watujiao, waje wanaojiamini,
Ziishe na ndoto zao, na usanii vijijini,
Twataka vitendo vyao, watatufanyia nini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Wajue matamanio, ya watu wa vijijini,
Kuwa na mipangilio, nani anafanya nini,
Isiwe maendeleo, hadithi ya maskini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Ni masoko tutakayo, kuuza hadi ugenini,
Nchi zituzungukao, tusiwe kizuizini,
Na yeu yote mazao, yafike bora sokoni,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Na yeu yote mazao, yafike bora sokoni,
Na wengine wauzao, tukutanie njiani,
Huko Kenya watakao, njia safi waachieni,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Msumbiji watakao, huru tuwe barabarani,
Zambia wapelekao, wasitiwe mashakani,
Rwanda na Burundi nao, iwe kama ni nyumbani,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Kongo wote watakao, wayaelewe mkoani,
Mpunga uulimao, si tu wa hapa ndani,
Si kosa yako mazao, kuuzwa huko mpakani,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Na kwa wingi wavunao, wapeleke Marekani,
Ulaya na nchi zao, wanunue duniani,
Uchina wayatakayo, tuuze kwa kujiamini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Ni yetu haya mazao, maji yatakayobaini,
Na ngano tuilimayo, umeme tutauwini,
Kahawa tuivunao, kuja jenga vijijini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Wenetu watotakao, ili kutafuta mjini,
Waanze kwa yetu mazao, biashara kusaini,
Wawwe wayapelekayo, kona zote duniani,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Na wanavijiji wajao, waishi kama mjini,
Pasiwe wayakosayo, eti waishi shambani,
Ila watu wang'arao, kwa siha pia imani,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Wanasiasa wa leo, hawatufai yakini,
Wataka ishi kileo, sisi twishi kizamani,
NI wao wajaliwao, sisi tuko taabuni,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Wajua shida tunayo, watununua kwa thumuni,
Hakika sisi vimeo, ila hatujajibaini,
Tugeuke ni walao, kura tusimpe mzaini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Wale na watu wao, kwetu wakose thamani,
Tuwe tuwachukiayo, duniani na mbinguni,
Tusiwape tarajio,ila wawe lawamani,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Na kura watuibiao, sheria tuzibaini,
Kukataa watuziao, kura kuwa ushahidini,
Hata wale watumwao, na dola ilio mjini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

Demokrasia iwe kwao, inaishi vijijini,
Tuwe tuwaondoao, wafanyao uhaini,
Tupitishe maazimio, vinara bora kuwini,
Twataka maendeleo, si hotuba vijijini!

No comments: