Wednesday, November 30, 2011

Vijana wa Tanzania

Vijana mnatumiwa, wazee kuwainua,
Nyuma mnabakia, makombo mnayapewa,
Wakati umefikia, usukani kuutwaa,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Vyama sasa vyawagawa, kutawala iwe poa,
Nanyi hamjajua, madebe mwawapigia,
Akili zikikomaa, kando mtawafagia,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Yenu hii Tanzania, ya wazee haijawa,
Ima fa ima kuamua, nchi kuisimamia,
Wazee wameshapoa, akili zinalemaa,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Maamuzi wachelewa, haraka yanayofaa,
Tanzania kuongoa, juu ikaja kupaa,
Vijana mnatakiwa, vitani kuja ingia,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Bungeni wanaosinzia, lazima kuwaondoa,
Hatimaye kubakia, uangavu walokua,
Fikra kuzichangia, bora tukaja jaliwa,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Vijana wa Tanzania, uchama kuukataa,
Jumuiya yenu kuwa, ya vijana Tanzania,
Uchama mbali kufia, umoja tukaulea,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Nguvu zitawazidia, chini ya chama hupwaya,
Mengi wanayoamua, ni wazee yawafaa,
Na si kizazi kipya, ambacho hufikiriwa,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

Nyie wazazi mshakua, kizazi kinachojia,
Balaa kuwaondolea, mwapasa mengi kujua,
Salama nchi ikawa, hata mtapojifia,
Vijana wa Tanzania, kuweni kitu kimoja!

No comments: