Balaghamu zinafaa, mvuke kuuachia,
Watu wakija kupoa, hasira huwapungua,
Maandamano yafaa, ni valvu maridhawa,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Balaghamu kipungua, watu huja fikiria,
Wakiteta watajua, lipi la kutarajia,
Na hatua kuchukua, tatizo kuliondoa,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Kelele zikipungua, maneno huyasikia,
Ujumbe ukaujua, na kazi kuufanyia,
Shida kutatuliwa, amani ikarejea,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Haya anayezuia, bomu ajilipulia,
Si leo si kesho jua, siku itajafikia,
Na wote mtajalia, bila mtu kubagua,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Ondokaneni na ujuha, mikutano kukataa,
Hiyo si demokrasia, nchi itajakuvia,
Na ushindi mkipwaya,hamwezi chaguliwa,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Ujinga mkiulea, mkaa mwajipalilia,
Vijana kuwanyanyua, waende kuangalia,
Dhiki kujazigungua,haraka kuziondoa,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Hatua mtatembea, watu kuwaaminia,
Kesho kuwategemea, mtaja kuja wasaidia,
Nalo hili wakijua, mtaibadii nia,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Ni vingi mnachukua, mwala na kubakishia,
Pipani mnatupia, wengine walala njaa,
Haya mkishayajua, nchi upya huzaliwa,
Balaghamu za wananchi, huisha kwa maandamano.
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment