Monday, November 14, 2011

Bilauri

Menginey bighairi, ufanisi kuchagua,
Hakuna linalojiri, ila kwa kupiga hatua,
Na waliotasawari, hili vyema walijua,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Mwenye kutafuta kheri, daima utamgundua,
Namna anavyofikiri, ni nusu imepungua,
Na shari mkusudia, ni kabisa haijajaa,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Kudra mwenye hiari, Mola atamwangazia,
Ismu haachi kariri, njiaze anamopitia,
Ilmu ataviinjari, na dahari si dunia,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Ilmu atavinjari, Alamu keshamwambia,
Hili kwake si ghururi, ni ndia iloandaliwa,
Abadani si kafiri, kukufuru anojua,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Na wengine hushauri, kutopotosha kujaa,
Mithili huikariri, nusu kitu kimejaa,
Ni rahisi kufikiri, ila gumu kutumia,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Ingelikuwa safri, nusu njia kufikia,
Atazituma habari, fikio akaribia,
Inshallah kwa saburi, hatimaye kuingia,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Ingekuwa utajiri, upungufu hatojua,
Atamsifu Qahari, kitu hajapungukiwa,
Ni mzima wa bukheri, na mengi kamjalia,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Mtawala hudhihiri, Muumba kumwangukia,
Na kila akifikiri, hutosheka alopewa,
Ukubwa ataghairi, zaidi akakataa,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

Iweje kwangu mshairi, hili kutolitambua,
Tayari nimeshakiri, jambo kulikubalia,
Sio ya kwangu dhamiri, ukweli kuupindua,
Nusu tupu bilauri, au nusu imejaa ?

No comments: