Monday, November 14, 2011

Wawakilishi hatuna

VYAMA huwa vyachukua, na wabunge wakwapua,
Ili fedha kujazia, kura wende zinunua,
Mwasema mmechaguliwa, kumbe mmejichagua?
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Afrika ililaniwa, na sasa inalaniwa,
Mweupe keshapangua, mweusi ameingia,
Mkoloni nawambia, sio rangi kutambua,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Lengo lao kulijua, ukubwa kutoachia,
Wako tayari kuua, madarakani kubakia,
Na wizi wanatambua, ndio unaowasaidia,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Katiba watapindua, kwa hila kuzitumia,
Wananchi kuwahadaa, mbumbumbu wasiojua,
Jambo hili wamejaliwa, huwezi kuwafikia,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Afrika yaugua, maradhi yasotibiwa,
Na wanayoyachangia, viongozi walokuwa,
Kisa uroho na tamaa,mamlaka kung'ang'ania,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Nchi wanailangua, na haki wazichukua,
Na mabunge yamejaa, watu wa kuteuliwa,
Ili kuja kutumiwa, siku inayochaguliwa,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

Muumba wetu radhia, tuangalie raia,
Ni wewe unayetwaa, na pia unayetoa,
Kikombe kutuondolea, mikosi kuikimbia,
Wawakilishi hatuna, wa wananchi Afrika.

No comments: