Sunday, November 13, 2011

Mfumo uliofumuka

Mfumo uliofumuka

Kwa waliokwishajaliwa, kuchunga kazi twajua,
Hili wanalolielewa, huzichukua hatua,
Mfumo kuuangalia, na kuufuma upya,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Mfumo ulioachia, huvuja na kusinyaa,
Mizani inatakiwa, kutozidi, kutowia,
Na hali ikitulia, basi lengo hutimia,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Kuushona upya, sasa tunashauriwa,
Ni vyema kuzingatia, na wasia kutumia,
Mambo kutoteketea, tukaja kuyajutia,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Ushoni kujifanyia, kwa mfumo tulofumua,
Kulaumu haijawa, itakayotufaa dawa,
Muda twajipotezea, hili kamwe halitakuwa,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Lawama kubambikizia, si mujarabu tabia,
Huna unalovumbua, ila karaha na udhia,
Na chuki ukiibua, kisasi kinakomaa,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Someni saikolojia, macho mkayafungua,
Ujinga mnaolea, ujanja mkidhania,
Wilaya pia mikoa, ukuu wanaopewa,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Wewe unayachimbua, watu wataka chimbia?
Wewe unayaibua, watu wataka fukia,
Na lini ilishakua, mgeni mwenyeji kua?
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Kuiepuka kadhia, ufungamano ni dia,
Mkoa utajavia, ukayakosa radhia,
Vijana wakachukia, wafanze yasiyofaa,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

Busara kubwa silaha, inashinda nyuklia,
Kuikosa ni hatia, nchi huweza angamia,
Heri wanaosikia, huziepusha balaa,
Mfumo uliofumuka, kwanza ufanyie ushoni.

No comments: