Sunday, November 27, 2011

Waziri mrembo?

Ni nani aliyekuwa, mrembo kwenye dunia,
Waziri alojaliwa, uzuri kuuchukua,
Sifa kummiminia, apite kwenye jukwaa,
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Mamissi tunawajua, cheo wanazawadiwa,
Twataka waliopewa, na nafasi kuchukua,
Jukumu walitumia, na wajibu wamepokea,
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Katika hii dunia, nchi ipi kutokea,
Afrika au Asia, au pengine Ulaya,
Ili tupate kujua, nchi iliyojaliwa,
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Ni mweusi atakua, au mweupe mzawa,
Kusini watamtoa, au kaskazi kua?
Magharibi kazaliwa, au Mashariki dia?
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Dunia kaifanyia, nini kilichomnyanyua?
Na ukimlingania, kitu gani kazidia,
Wenzie wamsifia, au wanamuambaa?
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Sura yake yavutia, na macho amejaliwa?
Ngozi laini kapewa, hariri kumithilia,
Na sauti ni ya hua, au kunguru amepewa?
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

Tunataka kumjua, na vipi kutuagua,
Ujinga kuja jivua, na ufakiri kutua,
Ya heri kutunukiwa, malau tukaambaa,
Ni nani waziri mrembo, shindano kimataifa?

No comments: