Wednesday, November 30, 2011

Nimeshakata tamaa

Tamaa imepotea, wengine nawaachia,
Labda kuwasaidia, usia najiandikia,
Muda ukijafikia, malengo kujifichua,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

La kwanza kuwaambia, dira imepinduliwa,
Vyama vimechukuliwa, na watu wenye tamaa,
Ukubwa wanauwania, na kazi hawajaijua,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

Waingia maharamia, wafuasi watolewa,
Sasa walioshikilia, mradi umeshakua,
Yao wanaazimia, ya wananchi wazimia,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

Wakubwa wanajifua, wanyonge wanafulia,
Shilingi inatitia, dola yazidi kupaa,
Bei zazidi kukwea, na lishe yadidimia,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

Mzee nimeshakua, ni yanini kukomaa,
Wanaotufuatia, mapambano kwendelea,
Ushauri nitatoa, watakaponiambia,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

Tungo wakijisomea, mengi pia kuyajua,
Wapi tulipopotea, porini tukaingia,
Nani wa kulaumiwa, mwema aliyedhaniwa,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

Mola tunamuombea, apange kumuumbua,
Wote tuje kumjua, awe kwenye historia,
Vizazi kumzomea, na moto kumwombea,
Nimeshakata tamaa, kazi kwa kizazi kipya!

No comments: