Sunday, November 13, 2011

Kiumbe msahaulifu

Sisi ni watu dhaifu, anatujua Muumba,
Haiwi yetu sharafu, kwa lolote kujatamba,
Ila kwa lake Raufu, alilokwishakuliumba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

Katupa yetu tarafu, sikuzote kumuomba,
Hadhiye ni kumsifu, na wasifu kuuimba,
Akatufanya arifu, dunia tukairemba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

Dua ni wetu mkufu, sio kitanzi cha kamba,
Wengi wanajikhalifu, kumkimbia Muumba,
Wakakosa uongofu, kwa uovu wakatamba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

Hainipungui hofu, nikimkabili Muumba,
Namjua yeye Chifu, wengine wote washamba,
Kura yangu ya turufu, kwingine sintaikomba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

Nauomba unadhifu, niepushe na mapumba,
Niupate usharifu, viumbe ulioumba,
Sote pamoja kusifu, vile ulivyoviumba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

Tucheze pia madufu, na kaswida kuziimba,
Ewe mfufua wafu, utupe ingawa chumba,
Firdausi shaufu, kama tukikosa nyumba,
Mja msahaulifu, kumbuka yupo Muumba.

No comments: