Monday, November 14, 2011

Sheria isoandikwa

Laanatullahi kua, jamii wanaohadaa,
Hata Kurani yatoa, mwongozo sahihi kua,
Kuandika yafaa, ushahidi manufa,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Haki wanaoziua, kuandika hukataa,
Siri watawaambia, ili wapate kwibia,
Hili nani hajajua, ila walo makataa,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Kila jambo inafaa, kimaandishi likawa,
Vinginevyo kutania, tena mkubwa mzaha,
Wajua wanasheria, baadhi wajisheua,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Cheo wanakitetea, binafsi manufaa,
Ila sio Watanzania, kikweli kuwakwamua,
Isoandikwa sheria, mahakama hukataa,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Mazingira waandaa, utata unaozua,
Mafuu haya wajua, sembuse wazima walokua?
Hekima kuzingatia, yaliyokwishajaribiwa,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Twashindwa kuwaelewa, vyeo waliotunukiwa,
Akili watuchezea, kama wanaotumiwa,
Au shaitwani raia, mshauri mkuu kawa?
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Misahafu kuchukua, na kanuni kuzijua,
Karne yanukuliwa, visa na mikasa pia,
Ubovu wanaoujua, pua walishaangukia,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

Nchi yetu yapotea, arijojo imekua,
Nani kuifuatia, aweze kuiokoa,
Nahofu kubwa balaa, akili kutotumia,
Sheria isoandikwa, si sheria usanii!

No comments: