Wednesday, November 30, 2011

Sukari kwetu anasa

Swali ninawatumia, wanaojua sheria,
Soko huru imekua, au siasa nazaa?
Vipi mnayoamua, kinyume chake kikawa?
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Bei zote zatakiwa, zenyewe kujiamua,
Vipi mnaingilia, nini tulichoambua,
Si bora ingekua, mapema kuagizia,
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Soko huru mkitua, acheni likaamua,
Na bei itatulia, mbali mkiangalia,
Sio kulala ikawa, hadi jambo kutokea
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Mwakurupuka jamaa, bei kuitangazia,
Kichwani iliokaa, sio soko kuamua,
Kisha mnashangaa, mipakani kwelekea,
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Inawaona vichaa, mfanyalo hamjajua,
Ukweli mkitambua, afueni tutajua,
Rahisi inapokuwa, sisi twende kununua,
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Nje inapotakiwa, ni vyema kuiachia,
Mradi tumeshagundua, akiba ndani ikawa,
Ya nje tulonunua, hili tukitarajia,
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

Akili tukitumia, rahisi tukanunua,
Ghali yetu inapokuwa, wengine twawauzia,
Uchumi utajakua, biashara zikapaa,
Sukari kwetu anasa, soko mfungwa, soko huru?

No comments: