Wednesday, November 30, 2011

Umeme wanaolia

Habari toka mjini, umeme unawahini,
Ila huku vijijini, hatujui jambo gani,
Twashangaa kwa yakini, wanakosa kitu gani,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Umeme wao mjini, sisi hatujabaini,
GIza letu vijijini, japo miaka hamsini,
Washangaa duniani, wakitua vijijini,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Ni kisingizio gani, waweza toa mjini,
Kama huu uhaini, hauletwi na uhuni,
Miradi walobaini, mbona yote mashakani,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Nafaka wala njiani, na mbegu zi mdomoni,
Wamechoka wahisani, malengo hawabaini,
Twashangaa kitu gani, na shetani yumo ndani,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Shetani ndio wahuni, ya k wao wanathamini,
Hawajali vijijini, kila kitu kuwahini,
Ni maendeleo gani, mbona sisi hatuoni?
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Na wengine hayawani, wataka tuliamini,
Jambo lisilo makini, wala ukweli huoni,
Hatujawa majinuni, uongo kuuthamini,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

Mapinduzi ni auni, tukatazame Japani,
Wanarudi vijijini, wamechoka na mjini,
Na sisi tuwe njiani, kuthamini vijijini,
Umeme wao mjini, giza letu vijijini.

No comments: