Monday, November 21, 2011

Kwetu kukipendwa kwanza

Kujipenda tumeshindwa, vipi mengine kuweza,
Naona uongo twaunda, ukweli hatutaweza,
Utakuwaje mkandwa, na mgongo hujabanza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Vyaelea vilivyoundwa, iwe meli au meza,
Mjuzi aliyeshindwa, na siye anayeweza,
Na nchi bila kufundwa, majenzi haitaweza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Sio mtu wa kupendwa, vitendo asiyeweza,
Kwa maneno ni kiwanda, kila kitu hutengeza,
Bali kwa kutofundwa,vitendo hataviweza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Mwenetu akishapendwa, machungu atayaweza,
Akiki tukimranda, umma hatoupuuza,
Hulijua lipi ganda, na mbegu akaitunza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Kushinda kama kushindwa, ni mwanzo wa kujifunza,
Walozaliwa watenda, hili halitawachuuza,
Na hata ukimponda, kusimama ataweza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Mwana ataka kufundwa, malezi yasomkwaza,
Na Mwenyezi akimpenda, nuru itamwongoza,
Hatohitaji kupendwa, mambo makubwa kufanza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Twaona wanavyojipinda, na mengi hawataweza,
Adili wameisunda, wataka fanza uweza,
Muunda huwa muundwa, dunia kumchakaza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Wanasema wawapendwa, wale watakaowekeza,
Mzawa wamemganda, kila siku kumchuza,
Na wanawe wawakwinda, elimu wanawakwaza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Mola wangu kuwafunda, wanangu sintoliweza,
Wa mwanzo na mziwanda, Hafeez ninakutunza,
Walee unavyopenda, na wawe wenye kuweza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

Ni wewe wa kuwapenda, mimi hilo sintoweza,
Naomba changu kibanda, utawa kuja ufanza,
Na ibada kuiganda, tarafu ninayoweza,
Kwetu kukipendwa kwanza, ustawi utaanza!

No comments: