Wednesday, November 30, 2011

Mitumba ni hadhi yetu

Kunung'unika yafaa, wakubwa wameshaamua,
Suti mpya kuzivaa, ni wakubwa walokuwa,
Vizito wenye ridhaa, na vigogo nao pia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Mitumba wameamua, ni hadhi inayofaa,
Kwetu akina raia, ni lazima kuivaa,
Lawama haitafaa, twapasa kuitikia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Ni nguo tumeanzia, na sasa pia vifaa,
Meli watatuletea, mitumba zilizokua,
Ndege za kupaa pia, mitumba tutatumia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Magari yameshajaa, wala hayatapungua,
Matrekta yaja pia, na malori kununua,
Dampo nchi sasa kua, wakubwa wameamua,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Ajali zikitokea, mengine kusingizia,
Mola atatushangaa, kwa haya kuyaamua,
Jinsi tulivyozubaa, mikenge tunavyoingia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Mapato wamegundua, njia ya kujipatia,
NI kumi asilimia, watakayoichukua,
Roho zikiteketea, hayo yetu majaliwa,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Akili zimefubaa, twashinda jitengenezea,
Walau kuviungia, nchini tulipokaa,
Kwa zana kuagizia, na kuja kujiungia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Vya nje kutegemea, kamasi watatutoa,
Mbona watu wamejaa, na kazi hawajapewa,
Wazungu wanaojua, mitambo kujiundia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Ulaya tukisogea, wengi watatuitikia,
Kwetu kinachotakiwa, mishahara kuitoa,
Nyumba kuwapatia, waishi na familia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Wapenda kuogelea, pwani tutawajengea,
Mali ghafi kununua, kazi iliyobakia,
Kuunda wakaanzia, vyote tunavyohitajia,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Ustawi tutazua, tena fumba na kufumbua,
Tukazalisha vifaa, na nje kujiuzia,
Nyumbani vikazagaa, mradi umeme kufua,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

Tuacheni kuzubaa, nafasi hii sawia,
Twashinda ipalilia, au hatujaitambua,
Wengine wakigundua, fursa itapotea,
Mitumba ni hadhi yetu, wakubwa walishaamua!

No comments: