Monday, November 14, 2011

Mitumba ya nguo, sasa eropleni...?

Hamsini kutimia, Tanzania twaendelea?
Au nyuma twasogea, hili bado sijajua,
Lakini ninachokijua, gurudumu lakataa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Mkoloni kachukua, akili zilizobakia,
Badala kujitambua, sasa tunajiumbua,
Badala ya kuvumbua, sasa twaanza fukua,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Elimu zimepotea, ujuzi wazidi via,
Tunachojitengenezea, ni wizi wa kubakua,
Nalilia Tanzania, kaburini kujitia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Watu wetu twawajua, vibovu walishanunua,
Na mikataba wakatia, vilivyokuwa vya hewa,
Ikiongoza sanaa, nchi jangwa hubakia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Wapo watu wa dunia, kazi hawajaajiriwa,
Vitu hivi wanajua, kutengeza kwa hatua,
Letu kuwafuatilia, ajira kuwapatia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

KIsha elimu kuzua, yenye mengi manufaa,
Iwe inayodhamiria, kitu kututengenezea,
Kitu hicho kikifaa, nchi itazidi jongea,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Haya yote ni nazaa, mitumba kuinunua,
Hapa twatangazia, MV Bukoba nyingi kuzaa,
Na Spice Islander pia,maelfu kuuawa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Ndege juu zikipaa, za mtumba zitakuwa,
Kama Kongo itakua, kuanguka na kuua,
Kilio kikubwa kuwa, na laana kusambaa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Hawa wanaoshupaa, lao wanaliazimia,
Huenda twajipalia, wa moto mkubwa mkaa,
Na hao kujivunia, pasenti wanazojua,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Mabomu tutauziwa, ya Mbagaala kumbukia,
Ila haya yatulia, mpaka ukitumia,
Kisha huharibikiwa, kisha kuchanganykiwa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Sheria tunazijua, kwa tunavyozi pindua,
Hawana la kutwambia, mkenge weshatutia,
Mikosi twaingojea, na misiba na balaa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Ni heri ukazaliwa, taahira ulokuwa,
Kuliko Mtanzania, rahisi kumhadaa,
Na kimya kutulia, hata mauti kumvaa,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Vyuo vikuu vyajaa, nini wanachosomea,
Kutengeza wasojua, hadi mtumba kununua?
Dunia yatushangaa, mizubao tulivyokuwa
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Fisadi wafurahia, mavuno wategemea,
Na kampuni watazua, zingine zitoke Ulaya,
Watoto walikokuwa, na makuadi kutumia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Historia twangojea, kuja kutushuhudia,
Bure kulialia, wakubwa wameshaamua,
Mungu atawaangazia, ya kwake kuwatunukia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

Na kinachofuatia, kizazi nasikitikia,
Mzigo kuuchukua, vifaa vilivyochakaa,
Kama reli ilivyokuwa, na zetu za simu njia,
Tulianza mumba nguo, sasa hata ndege pia !!!

No comments: