Wednesday, November 30, 2011

Mwanakijiji si mtu

Ukweli hatujathubutu, ila tutasema nini?
Wa shambani sio watu, watu wakaa mjini,
Hii ndio nchi yetu, na huu wetu utani,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Hii ndio nchi yetu, na huu wetu utani,
Vijiji vyetu misitu, tena waishi gizani,
Wangelikuwa watu, huu si uhayawani?
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Nitawachukiza watu, walio serikalini,
Hilo kwangu sio kitu, ukweli watabaini,
Maana hawa wenzetu, hawakuzaliwa mjini,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Huu ubaguzi wetu, kama Afrika kusini,
Twasahau watu wetu, kama sio hesabuni,
Twadhani eti si watu, wanaoishi vijijini?
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Kujiumbua wenzetu, ubaya wala sioni,
Haufai utukutu, haukubali Manani,
Na maisha ya wenzetu, si pungufu kwa thamani,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Mtu hajawa kiatu, ingawa kina thamani,
Mtu hakika mwenzetu, hata awe masikini,
Na maendeleo yetu, bila yeye mashakani,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Mtu awe na ukurutu, bado anayo thamani,
Na wewe wala si kitu, utaenda kaburini,
Utaacha kila kitu, naye angali duniani,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Moyo ukiachwa butu, hushusha watu thamani,
Na akajiona mtu, ni ka-Mungu duniani,
Wawe watumwa wenzetu, na wakubwa majinuni,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

Iwe ni nuksi kwetu, makosa kutobaini,
Tuitoe toba yetu, atusamehe Manani,
Tuwapende watu wetu, kama ni wetu mwandani,
Mwanakijiji si mtu, watu waishi mjini!

No comments: