Thursday, November 10, 2011

Hayuuchi sultani

Jicho halina pazia, mtoto keshabaini,
Hadharani analia, hana nguo sultani,
Wakubwa wajishangaa, kavaa waliamini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!


Mwanasiasa kwingia, hoja akaibaini,
Akasema mwakosea, hayuuchi sultani,
Ila nguo hajavaa, mnapaswa muamini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

Hoja ikazingatiwa, sababu haijulikani,
Mkubwa kashikilia, kuona si kuamini,
Na wenzake kuchangia, ubishi kuwa imani,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

Na hapa ukifikia, nenda kalale nyumbani,
Uongo utauvua, si samaki baharini,
Au kuja aminia, jua ni Mungu makini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

Njaa inatuumbua, uwongo tunaamini,
Ukweli twaukataa, wengine kuwa wahaini,
Ama stua ntakustua, utandawazi wawini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

Mkenge tunshaingia, si watu wenye thamani,
Mashaka tunatiliwa, kama vile afkani,
Hoja zimetupotea, moyoni tunabaini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

Yatusuta historia, si tena aliamini,
Ni watu tusiojijua, rai zatoka mwilini,
Na jangwani kinakua, kilichomo akilini,
Hayuuchi sultani, ila hajavaa nguo!

No comments: