Sunday, November 27, 2011

Daktari mzuri

Daktari kali njaa, rushwa anaipokea,
Mwanasiasa shujaa, mwenyewe kauchukua,
Mshahara kachukua, mnono uliokua,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

Hadithi yafanania, ugali anayepakua,
Mwingi kajipakulia, kiongozi alokua,
Na waliobakia, kidunchu wanapewa,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

Mchuzi wote katwaa, wengine warumangia,
Kichwani kaazimia, yeye ndiye wa kufaa,
Wengine kwake mzaha, tena waliolaniwa,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

Ubinafsi wamjaa, kiongozi hajajua,
Aone yote ni sawa, akili anatumia,
Nchi inadidimia, wa kwake bado wapaa,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

Daktari kachakaa, kashindwa kuvumilia,
Shindanoni kaingia, ukweli wake atoa,
Wenyewe kujitibia, mimi Ulaya napaa,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

Daktari mwenye njaa, vipi kifo kuzuia,
Mwatutakia balaa, zahanati wakijaa,
Roho watajatutoa, nakisi kujizibia,
Daktari mzuri nani, shindano kimataifa?

No comments: