Mhandisi mlimbwende, atafutwe duniani,
Asiye shoga na mende, na mzuri wastani,
Na dunia imgande, na kumtunuku thamani,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Kama yupo na aunde, tuvitakavyo nchini,
Tuache kuwa vibonde, wa wazungu duniani,
Ardhi yetu itande, kwa tulivyovibaini,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Magari nani aunde, yatembee majiani,
Meli nazo tuzipande, kwenda nazo visiwani,
Na mitambo tuichunde, migodini na viwandani,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Ndege nazo tuziunde, za mizigo na liinsani,
Ziruke hadi ziende, kwa wetu hao watani,
Viongozi wazipande, waende ughaibuni,
Viongozi wazipande, waende ughaibuni,
Sio za watu wagande, kwa nauli maaluni,
Na wenyewe wawaponde, wawe hawana thamani,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Vyeti lazima vivunde, ubora umkononi,
Injinia tuwapende, waundao vya thamani,
Tena mema tuwatende, watupeleke angani,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Na milima na mabonde, tuyaambae nyikani,
Mbele tusonge kipande, chakuridhisha moyoni,
Na dunia itupende, kutupa mpya thamani,
Mhandisi mzuri nani, shindano kimataifa?
Sunday, November 27, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment