Wednesday, November 30, 2011

Lishe

Aipate lishe nani, bei kama eropleni,
Zapaa juu angani, na sisi tungali chini,
Walio na afueni, wote hao wa mjini,
Lishe aipate nani, bei zapaa angani?

Bei zetu mumiani, damu zanywa miilini,
Tumebaki hamnani, ni mashine za Manani,
Naye ni kwayo imani, uhai ungenda mbweni,
Lishe aipate nani, bei zapaa angani?

Hili jambo la kanuni, si bure hulibaini,
Lataka kwa yumkini, taratibu na hisani,
Na sio uhayawani, wengine kutothamini,
Lishe aipate nani, bei zapaa angani?

Ukiwaacha maaluni, wasio nayo imani,
Wao hawana utani, ubaya watasaini,
Na roho ziwe shakani, mijini na vijijini,
Lishe aipate nani, bei zapaa angani?

Naamini, siamini, mpaka uone ndani,
Maisha ni kitu gani, kama hayana thamani,
Na kudhibiti ni nani, ila walo mamlakani?
Lishe aipate nani, bei zapaa angani?

No comments: