Sunday, November 27, 2011

Mkubwa hasemi uongo

Wazee wamenambia, radhi napaswa kutoa,
Wadai nimekosea, mkubwa kumdhania,
Wao wanavyoelewa, haiwi linalodaiwa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Hilo nimezingatia, naapa kutorudia,
Sasa nimeshalijua, sintalizungumzia,
Kauli nitaitumia, kulingana ilokuwa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Uongo hatotumia, ukubwa alojaliwa,
Ila aliyelaaniwa, na wanaomfuatia,
Ila nilivyoambiwa, mkubwa huongopewa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Na wanaomwongopea, ajenda hatoijua,
Hadi chali amekuwa, au kutokujitambua,
Pale akiambiwa, pembeni sasa sogea,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Ukubwa juu hupaa, chini muhali tembea,
Na wanachokitambua, ni kula pia kupewa
Mikononi vikijaa, adimu kujitambua,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Watu tumbo kuchumia, ndivyo walivyozaliwa,
Ya wengine kuwasumbua,hayo hawakuzoea,
Ubinafsi huwajaa, kuzidi hayawania,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Hao wanaomsadia, ndio wanaotuhadaa,
Ya kwao kujichumia, na nafsi kulindia,
Mkubwa wakamzidia,mikenge akaivaa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Ukubwa unapokua, vibarakala huzua,
Matumbo miungu huwa, yakaanza abudiwa,
Nafsi hubarikiwa, utukufu zikapewa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Kombakomba huzaliwa, kama kupe vile huwa,
Mwilini huning'inia, kwa wakubwa walokua,
Na wengine jibwa huwa, kumlinda alokuwa,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Hao ndio huchagua, lipi afaa sikia,
Na adha kumwepushia, mabaya kutosikia,
Mtu kipofu akawa, kwenye yake tasnia,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

Bubu na kiziwi hua,awe asiyeyajua,
Karibu yanayotokea, nayo ya mbali pia,
Dunia humpitia, yakama keshajifia,
Mkubwa huongopewa, abadani haongopi!

No comments: