Friday, November 18, 2011

Aliamini

Bismillahi Yaghanii, ubeti ninaanzia,
Ningali yangu makani, ya Karimu Ijumaa,
Hili nimelibaini, na sasa ninalitoa,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Nikiwa aliamini, siogopi kuchukiwa,
Kusema kweli imani, hidaya walojaliwa,
Atanienzi Manani, na pepo kuniridhia,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Nawajua duniani, wagumu wa kusikia,
Wataka niyaamini, kwayo wanayonihadaa,
Kunifanya majinuni, thawabu wakanifutia,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Urongo sintaamini, Mola ninamhofia,
Duni makazi motoni, milele nitakokaa,
Nikifa duniani, peponi milele kukaa,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Kufa hapa duniani, hai pepo ninakua,
Na hili nalithamini, daima kuzingatia,
Simwachii shetani, njiani kuja potea,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Waipendao amani, uongo waukataa,
Huwaweka mashakani, utulivu kupotea,
Tembeeni ulimwenguni, ukweli mtajionea,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Waliokuwa rahani, amani imepotea,
Na sababu wabaini, hadaa zilizidia,
Na ahadi za ubani, udi zisizoujua,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Nijalie maskini, aliamini nikawa,
Pamoja na hali duni, nikawa wa kuaminiwa,
Mwislamu wa zamani, mmojawapo ikawa,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

Niafikishe Manani, ya heri kunijalia,
Daima kuniongoa, nisje nikapotea,
Siratul kupitia, salama nami nikawa,
Siogopi kuchukiwa, kwa kuwa aliamini!

No comments: