Wednesday, November 30, 2011

Mjinga akijaliwa

Juzi halikuanzia, milenie latukia,
Ukubwa anayepewa, fala hujizungushia,
Wakao kumsifia, na wala si kumuongoa,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Ukubwa wanaolilia, kwa magambo nazo riha,
Akili waliovia, jipya wasilojua,
Bahau hujivunia, matofali ya kujengea,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Na yeye juu akiwa, nchi huiporomoa,
Ahadi nyingi hutoa, ila chache hutimia,
Si mtu wa kujijua, tao hajaigundua,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Huzungukwa na hadaa, ndani na nje mwake pia,
Taa kwao mshumaa,na tamaa ni kinaya,
Ukubwawe huutumia, machafu kuyawazia,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Mola kumgeukia, usanii hutumia,
Hujifanya wanajua, kumbe njia wapotea,
Nafsi haiwi ua, bali tunda la kuoza,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Huzungukwa na jamaa, njia wasiozijua,
Ni ng'ombe waloachiwa, mchungaji bila kua,
Na simba akitokea, kila mtu lwake huwa,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Vitabu vinatuambia, hakika mali hadaa,
Pia wake zetu baa, tusipokujaangalia,
Aidha na wana pia, Mola anaotujalia,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Muumini maridhia, mitihani huijua,
Kila akitahiniwa, maksi huzichukua,
Hatimaye hujinoa, kufaulu kujaliwa,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

Haya nawasimulia, kukumbushana ni nia,
Kumbusha tunaambiwa, wapo watakaosikia,
Faida kwako ikawa, siku ya kuhesabiwa,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

NInasujudu Alaa, Awali uliyekuwa,
Akheri mtarajiwa, uweze kunijalia,
Kuiepuka hadaa, salama hai nikawa,
Mjinga akitawala, werevu huwachukia!

No comments: