Wednesday, November 30, 2011

Nanywa tope

Kitu gani washangaa, tope nalimiminia,
Ndiyo maji yalokuwa, kijijini twatumia,
Ndivyo mlivyoamua, toka uhuru kwingia,
Waamua ninywe tope, kwanini unashangaa!

Dodoma tumezoea, Umasaini nao pia,
Maji yasiyotufaa, ndyo tunayotumia,
Serikali yashangaa, hali hili wamezaa?
Waamua ninywe tope, kwanini unashangaa!

Kunywa safi mwaamua, nyie juu mlokua,
Na kisha mnashangaa, tope tunapobugia,
Na hamjatufikia, japo tunawangojea,
Waamua ninywe tope, kwanini unashangaa!

Wadudu ni wetu pia, Mungua anatusaidia,
Anazilinda aya, vingine tungejifia,
Tunaowategemea, bure ghali wamekua,
Waamua ninywe tope, kwanini unashangaa!

Beti zimeshatimia, ujumbe nimeutoa,
Vingine kuangalia, au utu wapotea,
Vipi tutawafikiria, dhamana mnaopewa?
Waamua ninywe tope, kwanini unashangaa!

No comments: