Thursday, November 10, 2011

Aliyempenda chura

Mwanamali kasakura, turufu kaambulia,
Aiyekuwa ni chura, kumbe mwana maridhia,
Shetani alimpora, ufalme alopewa,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!



Na yake kubwa nusura, ni kupenwa ilikua,
Mitaani kuzurura, binti kamchangamkia,
Japo hakuwa na sura, binti hakumchukia,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Maisha yana tijara, kwa wengine ni izaya,
Na wasio na subira, hili hawajalijua,
Ukidekeza hasira, mwenyewe unajiua,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Hatuzijui ishara, na rahisi kuzainiwa,
Ikabaki ni hasara, kuwa watu wa kulia,
Ikhalifuni bendera, upepo mnaofuatia,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Yaniwahi madhukura, ikali sintojijua,
Na mimi mwana wa ghera, hatari sijakimbia,
Na hapo nilipogura, maisha nakimbilia,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Siwezi yangu kuchora, na yatakayofatia,
Nimeshaikosa dira, njia naweza potea,
Na kazi si kuzurura, hilo halitonifaa,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Ningeiomba shakira, uono kujipatia,
Nikajua kwa bashira, yatakayonitokea,
Ningejenga ngome imara, nisije kujavamiwa,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Mimi mja wa hadhira, karama sijazipewa,
Sitii yangu dhamia, ila yangu majaliwa,
Nijapo fanya ziara,huenda nikajigundua,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Na maisha ni halua, wanayoyavumilia,
Ukiendeshwa na hisia,pabaya itakutia,
Vigumu kuokolewa,ubinafsi ulivyojaa,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Na wengi waangama, dhahabu kukimbilia,
Kila kinachong'aa, thamani hukijazia,
Wakija shtukizia, wamekwisha umia,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

Binti yangu nakwambia, chura kutomwachia,
Huyo ndiye anayefaa, mjenzi mwenzi akawa,
Taratibu kidunia, ndio ifikayo hatua,
Aliyempenda chura, mwana mfalme kamwoa!

No comments: