Sunday, November 6, 2011

Baramaki

Baramaki simshiki, kama si baa, balaa,
Kubwa ni yake ashiki, kila pembe kujang'aa
Hata mtu 'kifariki, hutaka yeye sifiwa,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

Husaidia wenye dhiki, kwa riha si manufaa,
Na mazishi hushiriki, kujua alivyojaa,
Na harusi hudiriki, mamilioni kumwaia,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

Wagonjwa kwake bunduki, malengo kuyalengea,
Aonwe mwenye spaki,na machozi anatoa,
Utadhani ni rafiki,au ndugu amjua,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

Televisheni riziki, ya kwake kumwangazia,
KItuoni hawafiki, kusema atakataa,
Na redio marafiki, japo hana analojua,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

Wakubwa wake mkuki, nyuma huwafuatia,
Aonekane kibaki, rais mtarajiwa,
Kamwe kwao haondoki, mpaka mmemjua,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

Mtu huyu mamluki, ni vyema kumkimbia,
Si VX ni suzuki, idadi humzidia,
Si hariri wa kaniki, pale unapokujamjua,
Kiongozi baramaki, si kiongozi balaa.

No comments: