Hamsini inshapotea, na bado unangojea,
Hao waliokuhadaa, bado wawafuatia,
Ndugu unajizuzua, mkenge unshaingia,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Mkiani wabakia, katika hii dunia,
Thamani haujapewa, wala ardhi na vifaa,
Si mwekezaji mzawa, wewe zana kutumiwa,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Mafuu umebakia, nani wa kukutambua,
Ardhi wanaigawa, na madini kuchimbua,
Mali asili watwaa, mapori wakuachia,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Juha wanshakutambua, huna unaloelewa,
Historia walilia, ya kesho hujayajua,
Utandawazi nazaa, kaburini kukutia,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Bado unadhania, vyama vingi balaa,
Umoja waulilia, wenzako wautumia,
Na damu unatishiwa, utadhani hukuumbiwa,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Uoga umekujaa, hofu inakutania,
Hata dogo wapagawa, kama mapaka kulia,
Kaburini unshaingia, hali hai wapumua,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Mwenzetu ungangojea, wa mjini kukujia,
Misaada kukumwagia, nyumba kujijengea,
Hadhi ukiitarajia, kwa jinsi utavyong'aa,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Maji unayategemea, bombani kukumwaia,
Siku hiyo najutia,wewe hutakujaijua,
Bila peponi kwingia,au motoni kukwaa,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Umeme utaujua, kwa nyaya juu zapaa,
Bombani utasikia, wazimwa na kuzimua,
Taa yangu maridhawa, kijinga cha kuzubaa,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Barabara sio njia, nani kuja kukwekea,
Faida hawajaijua, bure watagharamia,
Na siku hukujaliwa, ni hasara kuingia,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Ni nani kuja kukaa, kijijini mwazubaa,
Afya imepotea, starehe ni mzaha,
Elimu mmelemaa, hakuna la kulijua,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Ndio maana twaamua, kusahau manufaa,
Limeni mtatuzia, hata kichwani kutwaa,
Njiani tutawapokea,kidogo kuwalangua,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Mola atawahurumiwa,kwa mateso mlivyojaa,
Pengine akisikia, nusura mtaijua,
Vichache kuwajalia, nanyi mkavikumbatia,
Kijiji kitajajengwa, ukishaaga dunia!
Sunday, November 6, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment