Ngedere jina kapewa, mwanasiasa wazua,
Hila ameshajaliwa, dhihaka pia hadaa,
Hata jambazi akiwa, mchamungu hujitia,
Mwanasiasa ngedere, hula vyako si vya kwake.
Vya kwako huvitumia, vya kwake hutatumia,
Huchukua asopewa, asikupe chakupewa,
Mwingi kusemea pua, wadhani ana mafua,
Mwanasiasa ngedere, hula vyako si vya kwake.
Shamba watalivamia, la kwao lisilokua,
Wakavuna na kutwaa, mazao yaliyojaa,
Wakayapelek kuliwa, wao na zao jamaa,
Mwanasiasa ngedere, hula vyako si vya kwake.
Haki watakuambia, walikwishachaguliwa,
Ridhaa wanshapewa, vya kwako kuvitumia,
Vya kwao ukisogea, roho watajakutoa,
Mwanasiasa ngedere, hula vyako si vya kwake.
Ngedere ndugu hajawa, japo sura kachukua,
Utu hakutunukiwa, ubinadamu kavia,
Tumbole huabudia, hilo ndilo analojua,
Mwanasiasa ngedere, hula vyako si vya kwake.
Thursday, December 1, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment