MAUDHUI zinavia, hali redio zinajaa,
Kila unalosikia. upuuzi unanukia,
Hekima imepungua, chapa waifikiria,
Wakiwapo redioni, hudhania wasikizwa!
Watangazaji kutua, ndilo wanalongojea,
Kibaya au chafuaa, hakuna wa kuchagua,
Wahariri wanapwaya, elimu hawajapewa,
WaKiwepo redioni, hudhania wafatiwa!
Redio zinazofaa, za nje kuzisikia,
Busara zinatumia, na elimu zinatoa,
Si wajinga walokua, wajanja wakidhania,
Wakiwapo redioni, hudhania wasikizwa!
Maboi watangazia, na hausigeli pia,
Redio zinadidimia, akili kutotumia,
Wachache wanaridhia, hicho kinachoandaliwa,
WaKiwepo redioni, hudhania wafatiwa!
Kusoma wanatitia, ajira wakimbilia,
Au vibarua kua, sauti kufurahia,
Hali kinachotakiwa, ubunifu watu kua,
Wakiwapo redioni, hudhania wasikizwa!
Wengine wanatumia, wazee wali9kua,
Mambo wanayojua, kupanga na kupangia,
Redio wakazifufua, TV nazo pia,
WaKiwepo redioni, hudhania wafatiwa!
Aljazeera tulia, BBC nayo pia,
Vipindi vinavutia, kuchoka hutosikia,
Ndivyo inavyotakiwa, kuiga na kuzindua,
Wakiwapo redioni, hudhania wasikizwa!
Zetu muziki zajaa, matako kubwabwajia,
Sasa ni kama kinyaa, tumekwishayazoea,
Yako wapi yenu mapya, tuweze kuangalia,
WaKiwepo redioni, hudhania wafatiwa!
Wednesday, January 4, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment