Wednesday, January 4, 2012

Titi la mama mzizi

Titi la mama ni tamu, tena ni lake malkia,
Kiswahili ni adhimu, wote twakizungumzia,
Dunia yakufahamu, ni ya sita kwa ukubwa,
Nchi haikukarimu, kwa kuwa macho wazibwa,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !




Ulimi wangu mzito, nyingine kuichambua,
Ila ingepewa wito, rahisi nyingine kujua,
Ningeufanya mkato, Kichina nacho kujua,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Ningeanzia utoto, wazazi kuwasumbua,
Lugha zisifanywe nzito, darasani kuelewa,
Tukacheza kiutoto, maabara kutumia,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Kiarabu cha mvuto, haraka ningekijua,
Kireno cha maliwato, nisingekihurumia,
Kifaransa cha mseto, nacho ningelikijua,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Maabara zenye wito, kila shule zingekuwa,
Na kazi yake mchakato, lugha kuzihudumia,
Kwa wote kuwa mvuto, na nyingi kuzielewa,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Madarasa si mseto, mengi kujichanganyia,
Ninasema kwa mkato, lugha ni kuziondoa,
Elimu hasa ni wito, darasani kuijua,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Kufundisha sio ndoto, maneno tutayajua,
Ukipita mchakato, dhana tutazielewa,
China kwao manukato, lugha yao watumia,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

Korea ni wao wito, video twajionea,
Lugha yaleta fukuto, vitu kujijengea,
Na kama si ya utoto, huwezi kitu vumbua,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

India kwao ni fito, utamaduni wakua,
Sisi twajipiga ngoto, wenyewe tunaumia,
Tunarithisha watoto, cha kwao kisichokua,
Titi la mama mzizi, vinginevyo haukui !

No comments: