KIFO hutushtua, hatima tukaijua,
Na kila mkumbushiwa, hili angezingatia,
Wangebadili tabia, kwa roho kuangalia,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Mtu upya huzaliwa, umauti ukitua,
Mbio kasi hupungua, nyuma akaangalia,
Na kisha akatulia, mwenyewe akajijua,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Haya wasiyoyajua, huweza kushangilia,
Adui 'kitangulia, sherehe akanuia,
Kumbe kesho naye pia, hukohuko huelekea,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Wale wanaojijua, hayati hana hatia,
Huwasamehe kwa nia, wakasahau mabaya,
Pepo kumuombea, ijapo kwa kupitia,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Huruma huwaonea, nyuma wanaobakia,
Nao wakifikiria, iko siku itakuwa,
Nao wakayoyomea, msaada wakatoa,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Mama umetangulia, wanao tunafatia,
Twazidi kukuombea, peponi kukubaliwa,
Msahama ukapewa, kwa uliyopungukiwa,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Maliki twamwangukia, uwezo kutupatia,
Kwa sadakati jalia, kwa wingi kukutolea,
Adhabu zikapungua, na thawabu kunyanyua,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Rabana yetu sikia, waja tunakulilia,
Sisi kwako tunajua, ni lazima kurejea,
Tuelekeze hatua, tusije potea njia,
Kifo kinapotokea, mja upya huzaliwa!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment