UKUBWA huu balaa, kila cheo kuchukua,
Makosa yazidi jaa, na madhambi yanakua,
Hapana kusingizia, ovyo mambo yanakua,
Kofia mnazovaa, zingine zawazuia!
Nyengine zimefubaa, kaniki zilizokua,
Rangi hautoijua, ila walokushonea,
Baadhi ni za vichaa, huokotwa kwenye jaa,
Kofia mnazovaa, nyengine zawafunika!
Hucheka wanaojua, kila wakikuangalia,
Huruma hukuonea, washindwa kukuambia,
Hutotaka kuivua, kuvaa umezoweya,
kofia mnazovaa, zingine za kuazima!
Zipo zilizoibiwa, na watu kuwaibia,
Laana zinachukua, kubeba wajibebea,
Na ukichanganyikiwa, mganga hutomjua,
Kofia mnazovaa, zingine za kusanzua!
Nyengine za kutania, zinazopima tamaa,
Ukubwa kuulilia, hata usiokufaa,
Uroho wakaujua, mwilini unavyotambaa,
Kofia mnazovaa, nyengine bure mzigo!
Mwashinda liona jua, na miwani hamjavaa,
Kisha mwawasingizia, miwani waliovaa,
Jua wamelipepea, mbinguni laenda paa,
Kofia mnazovaa, zingine zawazuia!
Juu mkiangalia, ya chini mtayajua?
Kofia zawahadaa, mwadhani mnyajua?
Macho hamkufungua, njia hamtaipotea?
Kofia mnazovaa, nyengine zawafunika!
Za kuazima mwavaa, hali upepo balaa,
Juu zikichukuliwa, hamwezi zikimbilia,
Watoto watazitwaa, na kwenda kuzichezea,
Fikirini kujivua, na chache mkabakia,
Hadhi mtajipatia, na ubora kuzidia,
Kubangaiza ikawa, kwenu nyie historia,
kofia mnazovaa, zingine za kuazima!
Watu sasa wamejaa, mambo yote wanajua,
Mkiweza kuchagua, jiniasi watakua,
Nchi kutochechemea, ustawi wakazua,
Kofia mnazovaa, zingine za kusanzua!
Machache nikijaliwa, yanitoshe kwa wasaa,
Kidogo yanapokua, moyo ndivyo hutulia,
Mengi yanavyokujaa, huachi kujaghasiwa,
Kofia mnazovaa, nyengine bure mzigo!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment