Sherehe lazima kua, mwana anapozaliwa,
Huzidi moja hatua, kizazi kinavyokua,
Warithi kujipatia, wasiyo nayo hatia,
Mwana anapozaliwa, kizazi chazidi kua!
Amani ndani hujaa, na upendo kuenea,
Nyota hushangilia, malaika kupepea,
Kumbe aloingia, salamu kumtolea,
Mwana anapozaliwa, kizazi chazidi kua!
Heshima humwamkua, mwanaadamu kaingia,
Salama alojaliwa, na tauhidi kupewa,
Vinginevyo kujakuwa, kiumbe kahujumiwa,
Mwana anapozaliwa, kizazi chazidi kua!
Baraka tele hujaa, daima kumzungukia,
Kwa amani kuja kua, na nafasi kuchukua,
Yote aloandikiwa, yaje siku kutimia,
Mwana anapozaliwa, kizazi chazidi kua!
Ibada akifanyiwa, na dua akaombewa,
Hulindwa na wateuliwa, hadi atakapokua,
Safariye kutimia, katika hii dunia,
Mwana anapozaliwa, kizazi chazidi kua!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment