Hugwaya wanaosikia, nchi masikini ikiwa,
Huogopa kuingia, ombaomba wamejaa,
Na wanaosingizia, vibaka wakawavaa,
Umaskini si sifa, nchi hudharauliwa!
Watalii hukataa, nchi hiyo kuijia,
Pengine wakachagua, palipo na majaliwa,
Masikini kubakia, zaidi ya ilivyokua,
Umaskini si sifa, nchi hudharauliwa!
Viongozi maridhia, kwanza huu huondoa,
Hata wakata wakiwa, watu wakawanyanyua,
Wakaondoa udhia, nchi kujakurubiwa,
Umaskini si sifa, nchi hudharauliwa!
Wajinga waliokuwa, sifa njema hudhania,
Kila wanakopitia, wakatamba kufulia,
Kigugumizi kikawa, wenyeji kuwashangaa,
Umaskini si sifa, nchi hudharauliwa!
Mabakuli hungojea, mwishoni kuja tolewa,
Kidogo wanachopewa, kwa wingi wakachopoa,
Miaka huishilia, nchi bado yadidimia,
Umaskini si sifa, nchi hudharauliwa!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment