Tuesday, January 3, 2012

Hata ukiwa rais

Afrika ukitoka, na Ulaya kuingia,
Wote mnafahamika, maskini mwaingia,
Rangi wakiangalia, nyani wote wana 'kia,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Dhahabu ukiishika, ni boi watakujua,
Kadhalika dala pia, mikononi ukivaa,
Vingine hutodhaniwa, fukara kasaidiwa,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Viranja huweweseka, majuu wakiingia,
Dubai wakishafika, pepo huikaribia,
Huenda kwenye maduka, akili zikaishia,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Huona yalotukuka, nchi ngeni wanapokua,
Vigumu wakafunzika, na hayo kuyaelewa,
Hurudia Tanganyika, hawana lilo jipya,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Wamesafiri miaka, ni lipi walichukua,
Mambo yanaharibika, safari zazidi jaa,
Nchi yabaki kichaka, talzi Ulaya zajaa,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Watu wasiojijua, ndiyo wanayojaliwa,
Wengine kuwasifia, ya kwao yadidimia,
Hawajui kutumia, watu waliojaliwa,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Msaada wanangojea, hata wanavyovijua,
Ulemavu umekua, tena ni balaa mbaya,
Wa akili ulokua, bado hawajajitambua,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Ali umeyasikia, usemayo narudia,
Nchi ikiwa dandia, njiani itaishia,
Na ndivyo ilivyokuwa, hamsini ilokua,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

Pia nawe takataka, kwa mzungu unakua,
Ukubwa unaoshika, thamani hutoijua,
Ila ufanye hakika, umaskini kuutoa,
Hata ukiwa rais, fukara huonekana!

No comments: