Tuesday, January 3, 2012

Ufukara unanuka,

Waliokwishasalimika, hawaijui karaha,
Umaskini unanuka, kuliko hata jeraha,
Ufakiri ukiwika, majogoo huduwaa,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Maisha hugawanyika, pasiwepo na furaha,
Wasiwasi hukushika, kila jambo kuhofya,
Ukakonda kwa hakika, kama mwenye njaa mbweha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Usiombe ushirika, ufukara ni usaha,
Haupati mamlaka, hupoka waheshimiwa,
Wayaibe madaraka, kwa kukuona ni juha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Hutumia kwa dhihaka, huo wa kwako ujuha,
Kama mbwa wakabweka, hofu moyo kukutia,
Usishike la hakika, wala kujua nasaha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Ya kwao hujafanyika, kwa kuutwaa mrabaha,
Ya kwako kuharibika, kama kichwani chawa,
Wakazidi kutanuka, wazidishe na madaha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Hawa ndio Waafrika, ujima wanaokataa,
Ubinafsi wajivika, ndugu bado wanahaha,
Si wanaoaminika, kuja kuipata jaha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

Hushauriwa kushika, yale yanayokufaa,
Uache shughulika, na yasiyokusaidia,
Nafsi ukishashika, nawe omba msamaha,
Haunukii wanuka, ufukara sio raha!

No comments: