Tuesday, January 3, 2012

Fakiri na ufakiri

Neno nimelisikia, na mimi nawaambia,
Fakiri anayekua, ukafiri huwa pia,
Vinginevyo minghairi, kamwe haitatokea,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Utumwa huuridhia, na watu akatumiwa,
Lingine kutosikia, njaa akaiangalia,
Uhuru ukimwambia, huona wamhadaa,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Fulana huzichukua, na mbunge akipewa,
Pilau anapoitiwa, wa kwanza hutangulia,
Bure huikimbilia, uhuru akaachia,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Wanawake nao pia, vitenge huvipokea,
Na khanga nazo pia, shahada wakazitoa,
Haki wakaiachia, na utumwa kuingia,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Ardhi wamejaliwa, thamani haijapewa,
Wameshindwa kutambua, ni mtaji ulokua,
Umoja wangeujua, milioni wangevua,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Madini chini yajaa, bure viwanja watoa,
Hili wangeligundua, fukara wasingekua,
Leo mifuko ingejaa, na hisa kuzichukua,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Mali asili waachia, wakubwa wanachukua,
Umoja wangelijua, hili lisingetokea,
Mchana wangewavaa, chao mapema kutwaa,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Njia hawajazijua, kodi nao kuchukua,
Mradi chao chafaa, wageni wakiingia,
Na wa ndani nao pia, cha kwao wakitumia,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Ukafiri mwauvaa, kwani hamjajijua,
Utajiri mmejaa, wengine wautumia,
Wakati wa kuamua, huu sasa waingia,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

Amueni kukataa, ufukara kuuvua,
Serikali kuamua, haki yenu kuitwaa,
Milki kuichukua, na thamani yake pia,
Fakiri na ukafiri, hakika kitu kimoja!

No comments: