MWANANCHI ukikosea, wabunge kuwachagua,
Walio wengi wakawa, chama kimoja wajaa,
Mwenyewe utaumia, kwa yatakayotokea,
Bunge la chama kimoja, rahisi kukudhulumu!
Pale unapochagua, acha chama kukijua,
Chagua anayefaa, kuja kukusaidia,
Kiongozi wa kufaa, na kazi anayejua,
Bunge la chama kimoja, rahisi kulaghaiwa!
Ubinafsi kataa, utakujakulemea,
Ndugu na wake jamaa,chaguo kuu likawa,
Pembeni mliokuwa, makombo mkatupiwa,
Bunge la chama kmoja, ustawi halilei!
Kiakili wanapwaya, si wa kufikiria,
Hujikurupukia, kusema wasiojua,
Wakapinga yakufaa, wakatae yanayofaa,
Bunge la chama kimoja, katu halinayo tija!
Wazuri wa kuzomea, bila kitu kukijua,
Ukweli huupokea, badala ya kuuvua,
Hoja kazi kuwazia, na kusoma wanang'aa,
Bunge la chama kimoja, rahisi kukudhulumu!
Daima hulaghaiwa, kwa vijisenti kupewa,
Wasijue cha kufaa, ila hongo kuitwaa,
Na kisha kuazimia, nchi yanayoiua,
Bunge la chama kimoja, rahisi kulaghaiwa!
Ukweli ninautoa, na wengi wanaujua,
Si siri iliyokua, kila mahala wajua,
Ni udhia imekua, tena ni kubwa karaha,
Bunge la chama kmoja, ustawi halilei!
Kitambo twavumilia, siku tunazingojea,
Ukweli wasiojua, taifa hawatofaa,
Hoja wanaoziambaa, balaa watutakia,
Bunge la chama kimoja, katu halinayo tija!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment