Mwenzangu ukizubaa, uhuru ukaachia,
Hakka nakwambia, utumwa utaingia,
Na bila ya kujijua, tena ukatawaliwa,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Uhuru wanaochezea, thamani imepotea,
Si bendera kupepea, bali kujitafutia,
Riziki ikaingia, na uchumi kunyanyua,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Kujiajiri ni njia, ukoloni kukaaa,
Utumwa kutoingia, udhalili ukakua,
Ukageuka mzawa, mkimbizi ulokua,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Umoja usipokuwa, rahisi kuzainiwa,
Watawala nao pia, wakubwa kuwatumia,
Hatimaye mjekuwa, na nje mwatawaliwa,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Ubunifu ukipwaya, rahisi kutawaliwa,
Vitu kutojijengea, mwakaribisha himaya,
KIsha hudharauliwa, daraja kuondolewa,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Asili msipolea, mkaiga yasofaa,
Marekani walokua, watumwa mkaigia,
Daima mtalaliwa, kuamka haitokuwa,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Utamaduni kukua, utumwa hautokua,
Yenu mkishayajua, uhuru mwajipatia,
Mageni kuyakataa, na yenu mkatumia,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Nimeshawahadithia, muhimu yaliyokua,
Sasa mnachotakiwa, kazi kuiazimia,
Nyuma mtu kutobakia, asili kuililia,
Uhuru ukiibiwa, utumwa unakujia!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment