Ukweli ukizuia, watu gizani wakawa,
Nafsi ukahofia, kukosa zake tamaa,
Mantiki kuivaa, mizizi isiyokua,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Leo dunia yajaa, ibilisi walokua,
Binadamu humvaa, mtu ukamdhania,
Uongozi wakatwaa, watu kuja wahadaa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Viumbe huwatumia, masikini walokua,
Njaa ikiwasumbua, vijisenti hujapewa,
Mambo kujiandikia, ukweli yasiyokuwa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Na wengine hukataa, ya kweli yaliyokuwa,
Kisha wakayachagua, uongo yaliyokuwa,
Hadhara kuiambia, ukweli wakaudhania,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Nuru walioishiwa, habari huzifukia,
Ukweli kuuzuia, wananchi kutokujua,
Mbegu wakajipandia, za kuja kujijutia,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Makala huzikataa, kweli zinazofichua,
Wakubwa kuwaridhia, uchafu chini ukawa,
Hawa wamelaaniwa, nusura twawaombea,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Serikali isokua, na adili za kufaa,
Uongo inayolea, na uzushi kuuzua,
Heshima kuigawia, kazi ngumu inakuwa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Na viongozi wambeya, yafaa kuwakataa,
Uzushi wanaozua, wengine kusingizia,
Nchi huipa mabaya, mbali kupatiliziwa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Nchi inayojaliwa, ya Mola huyahofia,
Ukweli wataujua, na uongo kukimbia,
Hawana la kuzuia, ila Mola yasiyofaa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Haki huizingatia, watu wote kuwafaa,
Upande kutoegemea, wala kuuonea,
Na hawa maashallah, pepo wameahidiwa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Si walioruhusiwa, viongozi walokua,
Madhambi kujifanyia, huruma wakaonewa,
Tofauti haijawa, kati yao na raia,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Serikali isofa, dhambi itaziachia,
Viongozi walokua, waogopwe kuambiwa,
Mabaya yakafukiwa, na ukweli kuuawa,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Chama kisichotufaa, dhambi hushabikia,
Na wabunge wake pia,watu hawatawatetea,
Na chama hujaachiwa, madhambi kujifanyia,
Ukweli ukiuficha, na wewe mrongo pia !
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment