Wazee tumeshachoka, vijana twawaambia,
Na wakati umefika, madaraka kuyatwaa,
Nchi zipate jengeka, heshima tuakijua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Rushwa wanaoridhika, mifukoni kuitia,
Au ukubwa kuushika, ili kuja kutumiwa,
Ni maafa kutufika, kukomesha inafaa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Hii ni yenu miaka, vijana wa Tanzania,
Filamu mmeishika, hamsini kufulia,
Haya yaliyotufika, kazi yenu kuondoa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Elimu mnateseka, nchini kujipatia,
Skolashipu washika, watoto wao kupewa,
Hakuna cha kueleweka, kuongoza mwatakiwa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Wazee wanaotosheka, kwa posho kuichukua,
Na kisha wakatumika, kama chafu vitambaa,
Wasiwe wenye mashaka, kila kitu kwitikia,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Viongozi wa kuweka, sasa tunawakataa,
Kuchagua tunataka, sio wa kuteua,
Njaa inayowashika, na watu kuabudia,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Viongozi wa hakika, sio wa kupachikiwa,
Lazima kuwasimika, iendelee mikoa,
Kama nchi kutawalika, na ajira kuzizua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Chama kimoja kushika, kila kitu kilokua,
Hili bora kulizika, na wengine kuchagua,
Nafasi ziwe hakika, kwa kazi wanaojua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Na wanaobabaika, maamuzi kuyatoa,
Si viongozi hakika, ila hawa ni bandia,
Watuchezea mahoka,kusambaratika ikawa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Viongozi tunataka, sitini wasiokuwa,
Akili zilojengeka, na sayansi wajua,
Mambo wanaoezeka, na sio wanaoezua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Wazee ngazi kushuka, ushauri kuutoa,
Vijana ni kuwasuka, nchi kuishikilia,
Demokrasia hakika, kila kona kukomaa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Balaa litawafika, mkato wanovizia,
Sasa mmeerevuka, njia za panya mwazijua,
Usalama twautaka, zahama kuiondoa,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Nchi yetu yasifika, rasilimali kujaa,
Wazee wadanganyika, rahisi kununuliwa,
Pensheni waitaka, uzee haujaingia,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Wengine waserebuka, badala ya nchi kufaa,
Mamlaka waloshika, nafsi wajisheua,
Wakosa Uafrika, wenzao kusaidia,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Wazee wenye hakika, ukitaka kuwajua,
Vijijini ukifika, hapo utajionea,
Wanaishi kwa mashaka, afueni kutojua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Wazee wa uhakika, mitaani wamejaa,
Hawana lenye fanaka, taratibu wajifia,
Wagumu kulalamika, njaa huku yawaua,
Uongozi haki yenu, vijana wa Afrika.
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment