Tuesday, January 3, 2012

Vitani nitapoitwa

Vitani waliokuwa, na sasa wanakimbia,
Vibaya wamezidiwa, rushwa inawahadaa,
Ufisadi wawakwaa, ya kwao tu kuyajua,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Chama kingelisikia, ningewapa nadharia,
Akili kuitumia, kubuni yanayofaa,
Nchi ipate kukua, na chama upya kuzaliwa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!


Nafsi zawatangulia, ya wengi wayahofia,
Ulaji wazingatia, uzalishaji balaa,
Wallahi nawaambia, siachi kuwaokoa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Ujinga uliowahadaa, maliasili kwachia,
Ufukara kututia, tajiri tuliokuwa,
Mengine nitasusia, wananchi kujakuwafaa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Maradhi wanaougua, nafsi kupendelea,
Na sasa wamezidiwa, vitani wanakimbia,
Papo ningewaumbua, kitali wakarejea,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Vita waliojitia, umaskini kutoa,
Kumbe wajichumia, na matumbo kuwajaa,
Nisingeliwahurumia, wangeliona jambia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!


Vitani waliojitia, washindwa teknolojia,
Haraka ningewatoa, na wengine kuteua,
Vita kuendelea, tushinde kiteknolojia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Maji wanaotusumbua, mitaani kumwaiya,
Nyumbani kutoingia, mama zetu kuumia,
Mateso ningelikataa, afueni wakajua,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Maziwa tungetumia, maji kujatupatia,
Kigoma yakaingia, na Ujiji nako pia,
Sumbawanga kuogelea, mjini wanapokua,
Maziwa tungetumia, maji kujatupatia

Umeme wasiojua, vijijini wakikaa,
Hilo ningeangalia, sio mjini tu kupewa,
Vita vingelienea, kila nyumba kuingia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Taka tungelizoa, umeme tukaufua,
Taka pia zikatoa, iliyo bora mbolea,
Na vingine kurejelea, majumbani kutumiwa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Reli zilizojifia, nazo ningezifufua,
Kigoma waache kulia, na Tabora nao pia,
Na kisha inshallah, Rwanda, Burundi kwingia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Utalii ungekua, hadi vijijini pia,
Hali kuinyanyua, kona zote zikafaa,
Maelfu kuingia, makwetu kujichimbia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Viwanda ningefufua, kwa vyuo navyo kuoa,
Uhandisi kuujua, kwa vitu kujijengea,
Miradini wakakua, na elimu kuizoa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Afya ningeifungua, milango isofunguliwa,
Vifaa kujiundia, raia kuwatibia,
Na wageni wakajaa, kuja hapa kutibiwa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Mishahara ingekua, kwa watenda walokua,
Wabunge kuwazidia, na daima kuenziwa,
Ujuzi waliokuwa, nao wakajibishia,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

Vyuo vingelisambaa, viote kila mkoa,
Na shahada maridhia, wanamkoa kutwaa,
Elimu inayofaa, mkoa ukaitoa,
Vitani nitapoitwa, haki kuipigania,
Nafsi nitajitoa, nchi kuisadiai!

No comments: