Subira inatakiwa, mchumba kumchagua,
Nyumba ukizivamia, pabaya utaingia,
Na ukishamchukua, majuto kwako ikawa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Mola anayemjua, na kiyama kutambua,
Dini aliyejaa, uchaMungu kuwania,
Na mme kumwangalia, na watoto nao pia,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Mapenzi anayejua, ni ibada nayo dua,
Si uhuni kuutia, kwa uhuni na zinaa,
Ni lebasi ya kuvaa, nawewe unamvaa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Kichwa anayetumia, mwenyewe kufikiria,
Bora zaidi afaa, mke nyumbani akiwa,
Moyo wanaotumia, haweshi kuwa vichaa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Heshima aliyejaa, hata nacho wasokua,
Wakubwa kusaidia, na wadogo nao pia,
Ikawa yake tabia, na sio kuigilizia,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Wazazi anayelea, yao kuwatimizia,
Vyema kuwaangalia, hata wazee wakiwa,
Utoto wakarudia, visingizio kuzua,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Kishake akawalea, kama watoto wakiwa,
Nao wakafurahia, na radhi kuwaachia,
Hili lazima kujua, kuja chini hutakiwa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Usafi mwenye kujua, uchafu akakataa,
Kufuma anayejua, na mapambo kutumia,
Chumba kukiangalia, kama hotelini kuwa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Kupika anayejua, mapishi yalotulia,
Usiwe nayo tamaa, nje kwenda kuhamia,
Afya kukuangalia, nawe ukamwangalia,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Mchache wa kuongea, maneno anayechagua,
Hekima aliyejaa, na busara kutumia,
Ushauri kukufaa, katika unayoamua,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Asiyependa umbeya, wajao kuwashushua,
Kuficha asiyejua, lijalo kukuumbua,
Ukweli akakwambia, na wewe ukalijua,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Ubunifu alojaa, na utundu wa mapya,
Nyumba kutosinyaa, kwa ukale kuzidia,
Na wana kuwalea, kwa kiteknolojia,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Vyombo anayeelewa, jinsi ya kuvitumia,
Akidhi kuvitumia, sio vije kumtumia,
Yakaifaa familia, badala kuizuzua,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Televisheni wasaa, nayo akaipangia,
Video kuzikagua, utu zinazoulea,
Na kompyuta pia, uangalizi ikawa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Apaswa awe ni ua, kunyauka lisokua,
Daima 'kiangalia, bado jipya linakua,
Ikawa yako furaha, milele inayokaa,
Mchumba wa kuchagua, sifa ninakutajia!
Tuesday, January 3, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment