Tuesday, January 3, 2012

Kinyamkera

Hakuna kinayemjua, upeopo wenye hasira,
Chochote hukinyanyua, mahala kinapogura,
Vizito huvipembua, na kuvitupa kwa ghera,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Hakijui kubagua, mashavu kinapofura,
Macho hujipofua, iwe kukurukakara,
Na wanaokitambua, urafiki huuzira,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Manowari na mashua, zikiwa mbali na bara,
Baharini hukimbia, lakini pasiwe dira,
Maji yakawavamiwa, na chini kwenda sowera,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Hali nikiiangalia, nahofu kinyamkera,
Hapa kikijaingia, hakuna aliye bora,
Wote tutasanzuliwa, nyuma ibaki athira,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Hao wanaosinzia, inabidi kuwachora,
Malale kuwaondoa, tuwachapeni bakora,
Mijeledi wakitiwa,watawajua fukara,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Kinyamkera balaa, akitakaye ni jura,
Kila kitu kinang'oa, nchi ikawa kipara,
Hili wanalolijua, huiogopa kafara,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

Afu humkimbilia, wapate yake nusura,
Hifadhi kuililia, katika yote majira,
Kinyamkera kuvia, na kwingine kudorora,
Kikija kinyamkera, zoa hakitachagua!

No comments: