Tuesday, January 3, 2012

Maana yake ahadi

AHADI sio mradi, keshatuonya Wadudi,
Unaweza kuritadi, ahadi ukikaidi,
Na waja bila idadi, huogopa kuahidi,
Maana yake ahadi, kuitimiza ahadi.

Haimpendezi Ahadi, kwa walio wake Abdi,
Ahadi kutaradi, ikawa kama nakidi,
Anachotaka Majidi, ni ahadi zenye sudi,

Ahadi huwezi nadi, na kuifanza mradi,
Malaika hurekodi, wakaifata abadi,
Na siku yake Hamadi, lazima itakurudi,
Kipimo chake ahadi, kufanikisha ahadi.

Kataa kuwa kafidi, hii si ya kwetu jadi,
Mwafrika kwa mihadi, habadiliki abadi,
Hutenda aloahidi, hadi roho ikirudi,
Maana yake ahadi, kuitimiza ahadi.

Ahadi zenye midadi, nafsi hazihimidi,
Ni ukubwa kula kodi, na watu wasifaidi,
Huikasirisha radi, kwa wote ikajinadi,
Kipimo chake ahadi, kufanikisha ahadi.

Waijuao fuadi, hukataa ukuwadi,
Katika huu mradi, huyatafuta ya Hadi,
Kuwaongoza ibidi, hadi ilipo ahadi,
Maana yake ahadi, kuitimiza ahadi.

Huikamata shadidi, kamba yake alrashidi,
Wakubali tauhidi, vingine wasijinadi,
Hujua kila mradi, hutoka kwake Mubidi,
Kipimo chake ahadi, kufanikisha ahadi.

Na uongozi jadidi, kutenda hauna budi,
UKubwa wa kufaidi, ya wengine kukaidi,
Ni kitu cha ukaidi, hautunzwi hata Iddi,
Maana yake ahadi, kuitimiza ahadi.

Atuangalie Badi, tuwe wake mashahidi,
Nemsi ziso idadi, mastakimu kufaidi,
Na waja waso hasidi, kuwapa wetu mradi,
Kipimo chake ahadi, kufanikisha ahadi.

No comments: