Tuesday, January 3, 2012

Ukilipenda waridi

Ulilipenda waridi, miba uwe nayo huba,
Uzuri ukifaidi, usihofu chomwa miba,
Na randi zikijinadi, kubali yake haiba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

Usifanye ukaidi, waridi ukilishiba,
Kumbuka yake nakidi, iwe ni yako akiba,
Kwa kila lililo sudi, halikosi na msiba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

Hulka hii baidi, njia huwezi kuziba,
Huzaliwa kujinadi, likiwa na yake miba,
Ua hili maridadi, amelijalia Toba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

Uzuri ni yake jadi, na ubaya si kuruba,
Hutia wengi madadi, watamani kuliiba,
Ili nao kufaidi, kilichomo marahaba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

Hujazuka magaidi, kwa inda wakakukaba,
Wakunyang'anye waridi, kwa ujanja na ghiliba,
Ukifanya ukaidi, mdomo wakakuziba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

Ni ua lenye mihadi, huyazidisha mahaba,
Huituliza fuadi, majonzi ikayaziba,
Viumbe waso idadi, haweshi ua kupamba,
Ukilipenda waridi, penda na yake miiba.

No comments: