Ni ucha Mungu na haki, dunia inachokosa,
Wanyonge tunadhihaki, hali yao twaijua?
Nafuu yao hamaki, na moto mwajiwashia,
Dunia inachokosa, ni haki na ucha-Mungu!
Mnataka wale keki, mkata hawajapewa,
Posho mnaziafiki, mwawazidishia ukiwa,
UOni mwaufariki, vipofu mmeshakua,
Dunia inachotaka, ni haki na ucha-Mungu!
Muumba hakasiriki, hadi mnyonge kuuawa,
Haya mnayoafiki, umauti mwatutia,
Kila mnachobariki, ni wizi uliokuwa,
Dunia inachokosa, ni haki na ucha-Mungu!
Afriti wajinaki, nchi wameichukua,
Madharibi na mashariki, yasoyao wachimbua,
Yanabaki mahandaki, kisha na wetu ukiwa,
Dunia inachotaka, ni haki na ucha-Mungu!
Shilingi hatumiliki, punde mmeichukua,
Safari yetu mikiki, twendako tunachelea,
Ninaona hatufiki, tulikokwisha ahidiwa,
Dunia inachokosa, ni haki na ucha-Mungu!
Shetani anashiriki, wengine kuwatumia,
Ubia kaumiliki, kila kona twajionea,
Balaa zikihakiki, hakuna wa kuzuia,
Dunia inachotaka, ni haki na ucha-Mungu!
Naichelea Iraki, Tanzania kuja kuwa,
Viongozi wanafiki, vibaya kutumia,
Wenyewe watabaaki, matanuzi kwendelea,
Dunia inachokosa, ni haki na ucha-Mungu!
Usiache tubariki, sisi tunaopotea,
Tuiepuke mikiki, tusiyoitazamia,
Umoja usifariki, masikini sana kua,
Dunia inachotaka, ni haki na ucha-Mungu!
Monday, January 2, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment