WAKITHIRI masikini, katika hii dunia,
Wa jana sio zamani, fukara wameshakua,
Ulaya na Marekani, kama Afrika wawa,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Nchi zimerizaini, majaribu wakimbia,
Na wasio na imani, wengine wasingizia,
Amani ni hatarini, na wengi hawajalijua,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Naamini majinuni, mbumbumbu wanaojua,
Hawana kitu kichwani, ila wanayoyadhania,
Wenda juu pia chini, ukweli hawajajua,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Kila mmoja yu ndani, chumbaani kajifungia,
Uongozi duniani, nchini unasinzia,
Wameikosa amani, wapotea ushujaa,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Ninaona walakini, nami ninawaudia,
UNO itioke uwani, barazani kuindia,
Wakutane duniani, watu kuyazungumzia,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Na madai ya zamani, upya kuyasikia,
Wazidi umaskini, wengine twawaibia,
Tujue namna gani, hasara kuzifidia,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Viongozi wa nchini, kadhalika watakiwa,
Mifumo kutathmini, unyonyeji ilokuwa,
Maamuzi kuauni, tofauti kuitoa,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Twaishi kama zamani, neema ilipokua,
Mkiambiwa oneni, macho mwashindwa fungua,
Unanyonga umaskini, na ovyo watu kuua,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Nafuu harakisheni, nchi itaangamia,
Wamezidi maskini, bei zinavyokimbia,
Hawana tena imani, wanung'unika raia,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Tajiri na masikini, ncha mbili za dunia,
Waongezeka nchini, wasonacho Tanzania,
Tumaini hawaoni, na wengine wapotea,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Wengine hawaamini, bado wazidi tanua,
Wananuna masikini, punde wapasuke pua,
Na hasira ikiwini, watajua wasojua,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Mikakati hapa nchini, sasa imeathirika,
Haioni afueni, fukra mtambulika,
Ila walo ofisini, ndio watajirika,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Raia hana thamani, wakubwa wasomjua,
Hali yake hayawani, nani wa kumtumia,
Kazaliwa masikini, hana kitachopungua,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Ndivyowanavyoamini, waliokwishajaliwa,
Fukara wa duniani, hilo hawajaridhia,
Waeema hadi kaburini, haki wataililia,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Amini usiamini, marehemu wanalia,
Leo tuko msibani, dhuluma kuwafanyia,
Nchi daima walaani, unyama uliokuwa,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Tunakuomba Manani, hifadhi kutupatia,
Uondoe Maaluni, dhulumati walokua,
Tuwapate waumini, weye wanaokuhofia,
Ncha mbili za dunia, tajiri na masikini.
Monday, January 2, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment