MJA hili zingatia, huna wa kukusaidia,
Mzima unapokua, yabidi kujiandaa,
Na ujapotindikiwa, yako kukusaidia,
Wengi uwawezeshao, hukuacha ubomoke.
Watu ukisaidia, hata nduguu walokua,
Sifanye kutegemea, watakuja kukufaa,
Wengi hukukimbia, yao wakaangalia,
Wengi uwawezeshao, hukuacha uteseke.
Kama njia hupitia, hifadhi unayotoa,
Jumla wakufikia, nyumbani wakahamia,
Nyuma hawatakujua, pindi wanapofanikiwa,
Wengi uwawezeshao, si deni hawakulipi.
Hata kukusalimia, wengine hukuambaa,
Ni mkoma unshakua, dhiki utawalilia,
Mikono juu nyanyua, si wao wanaotoa,
Wengi uwawezeshao, wachache hukukumbuka.
Ushirikina kataa, Mola kumtegemea,
Riziki hukugaia, na wana kuangalia,
Ulimi wako zuia, kuomba wenye ukiwa,
Wengi uwawezeshao, hawanayo shukrani.
Ya Ghaniyu asikia, na yote ajionea,
Naye namtamkia, malipo nayangojea,
Hao niliowafaa, na wangu nao kuwafaa
Wengi uwawezeshao, asante mdai Mola.
Wimbo ninamwimbia, moyo wangu kufungua,
Hali yangu kuijua, na dawa kunipatia,
Nao wanaomjua, hili wanalihofia,
Wengi uwawezeshao, hukuacha ubomoke.
Mikono nainyanyua, riziki kutarajia,
Asiniache mkiwa, nyikani nikapotea,
Mradi nilishatoa, bwana atanigaiya,
Wengi uwawezeshao, hukuacha uteseke.
Safari yaendelea, mwishowe anaujua,
Siwezi kudamkia, na yake kuhimizia,
Subira naitumia, silaha inayofaa,
Wengi uwawezeshao, si deni hawakulipi.
Karimu anayajua, mimi nisiyoyajua,
Msamaha nangojea, na huruma yake pia,
Huku namsujudia, kwa aliyonizawadia,
Wengi uwawezeshao, wachache hukukumbuka.
Asante ninaitoa, kwa wanaoniangalia,
Mola atawanyanyua, na pepo yenu ikawa,
Na wasionitambua, shukrani ninatoa,
Wengi uwawezeshao, hawanayo shukrani.
Ya Latifu maridhia, adui wake udhia,
Wajua cha kuchagua, pia la kuzawadia,
Njia umeziandaa, ilo njema twalilia,
Wengi uwawezeshao, asante mdai Mola.
Sunday, January 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment