KIMBELEMBELE ukiwa, watu watakushangaa,
Haya unayojitia, si yako yaliyokuwa,
Soni imekukimbia, aibu yakuambaa,
Shoo zako mtaani, huonwa ni hayawani.
Senti haujapewa, shoo unajifanyia,
Ndani sio wa kukaa, unavamia mitaa,
Hata usiowajua, watazamaji wakawa,
Shoo zako mtaani, mjinga usiyejua.
Punguani umekua, wala haujajijua,
Wajifanya unajua, kumbe wanakutumia,
Nguvuzo zinaishia, wengine kutumikia,
Shoo zako mtaani, hunacho cha kuringia.
Mama Huruma wazua, 'Red cross' maridhia,
Shida zinawakimbia, kila unapoingia,
Vya nyumbani wasanzua, wengine kwenda wafaa,
Shoo zako mtaani, jeuri ya masikini.
Mdomo umejaliwa, kupanga yasiyokuwa,
Huwezi chini kukaa, moja ukajijengea,
Ovyo wahesabiwa, ila haujajijua,
Shoo zako mtaani, ya kesho hujajiandaa.
Huruma nakuonea, ukosapo kujijua,
Juu unawapandia, wawezao kukunyanyua,
Upuuzi umekua, ila unavumiliwa,
Shoo zako mtaani, na nyumbani kunanuka.
Kila kitu walemaa, ila shoo kuzigawa,
Nini unachopatia, maishani kukufaa,
Naona unapotea, macho haujafungua,
Shoo zako mtaani, zitaisha kwa madeni.
Muda unaotumia, laiti ungefikiria,
Mapya kujifanyia, mbali ungelifikia,
Ufakiri wauvaa, huku unaangalia?
Shoo zako mtaani, bahau ukijijua.
Sunday, January 1, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment